Tuesday, August 20, 2019

Makala: kusudio la maisha ni njia ya mafanikio yako


Imeandikwa na Abdallah Wihenge | Dodoma


Siku kadhaa zilizopita nilipata fursa ya kumsikia moja ya wazungumzaji mashuhuri sana Chris Mauki katika ukanda wetu wa Afrika mashariki katika kipindi cha redio na alikua akielezea jambo juu ya kuwa na maono,mipango na kujituma  ama kujiongeza kwa kwenda hatua ya ziada katika mambo ya kimafanikio. Katika msingi wa maelezo ya mzungumzaji alielezea juu ya umuhimu wa kujitafakari na kujenga picha kubwa ya maisha yajayo na hii hainzii ukubwani ni jambo ambalo linakita mizizi tangu katika kipindi cha makuzi.
Kwa mantiki hii ni wazi kabisa wengi katika jamii nyingi za watu weusi wamekwishakawia katika kutekeleza makusudi ya maisha yao na wengi wanajikuta wanaongozwa na mfumo na kasi ya maisha na si wao ambao wanaoendesha maisha yao. Matukio na misukumo tu ya maisha ndo humfikisha mtu mahala Fulani ama pakubwa au padogo inategemea tu na ‘zali’ lake.

Ujasiriamali ni kichaka kipya cha kukimbilia?
Kulingana na hali ya maisha imekuwa utamaduni au mazoea sasa hivi watu kujificha kwenye kichaka cha ujasiriamali pale ambapo kila kitu kimekwenda mrama. Mfano kijana amesoma na akakosa ajira basi ataingia kwenye kichaka cha ujasiramali,mtu akapigwa na maisha vilivyo basi nae kichaka hiki humuhusu. Kwa maneno yasiyo rasmi tunaweza kuita ujasiriamali ni neno jingine la ukosefu wa ajira. Na mkwamo huu ni kiashiria tosha kwamba wengi ya watu katika jamii zetu  hawafahamu kusudio la maisha yao. Ni maelekezo na mfumo tuliopewa ama na wazazi,walezi au jamii juu maisha. Wengi ya wanajamii hawaishi maisha yao ndani ya kusudio isipokua mfumo ulioweka na jamii na familia.
Katika kukielezea kichaka hiki cha ujasiriamali na biashara, moja ya waandishi mashughuli wa masuala ya biashara na ushirika aliwahi kuandika “Kwa miaka ishirini iliyopita, anaelezea jinsi kila siku, zaidi ya mawazo elfu mbili hujaribu kuanzishwa kama biashara, lakini kwa mwaka mmoja, ni asilimia tano tu ya kampuni hizi zilizosajiliwa zinaishi na kukua”
Swali likazuka kichwani mwangu kwa nini sehemu kubwa sana inashindwa? Na katika maelezo yake mbeleni alieleza kuwa wengi huanzisha biashara au shughuli nyingine ya kipato kwa kusudio lisilokua rasmi yaweza kuwa ama kwa msukumo au kwa lengo la kuvuka kipindi Fulani cha maisha au msukumo toka kwa watu na kuaminishana kwamba aina fulani ya biashara na hapa sasa hufuatiwa na jaribio la biashara na si biashara.
Katika mazingira niliyoyataja hapo awali ni wazi kwamba wengi watu wengi hivi sasa hawana mpango,mkakati wala kusudio la maisha yao isipokuwa ni maisha yenyewe ndio yataamua wao wawe nini.

Kusudi la kuandika Makala hii fupi ni katika kuona ni kwa namna gani kuweka lengo la maisha kunaweza kukupa picha na njia ya maisha yenye mafanikio. Na ikumbukwe kwamba mafanikio si pesa tu, ni mkusanyiko wa mambo lukuki ambayo hayo tutaayandika katika Makala zitakazofuata.
Biashara, ujasiriamali na shughuli nyingine za kuendesha maisha ni matokeo ya shughuli za kusudio la maisha na uwepo wa mtu. Kila mmoja ni lazima ale chakula na kuishi maisha na vyote hivi havifanikiwi mpaka pawe na shuguli ya kuingiza kipato. Haiwezekani watu wote wakafanya shughuli moja ili kupata kipato.Kwa maana aina shughuli ya kipato hutofautiana kati ya mtu mmoja na mwingine. Kwa kuwa kila mtu ni sharti afanye kazi ndipo apate maisha ndio maana Makala hii imejikita kuelezea ujasiriamali na biashara katika mtazamo wa kufikia kusudio la maisha.
Katika umri Fulani wa maisha akili ya mwanadamu huanza kufikiria kwa namna gani ama ni shughuli gani mtu anaweza ifanya ili aweze kufikia malengo Fulani ya maisha au kujipatia kipato na kuendesha maisha.

Gundua kusudio lako la maisha sasa!
Kusudio la maisha huanzia hapa katika kuchagua nini cha kufanya na namna gani ya kufanya ndipo watu wengi hupanda kipando kisicho sahihi katika kufikia malengo ya maisha yao na kwa namna wanaweza kufanikiwa.
Kipando au njia sahihi ndiyo itakayomfikisha mtu pahala sahihi kimaisha, ila kushindwa kujua upo duniani kwa lengo gani au wewe ni nani basi kwako maana ya maisha itabaki kuwa ni pumzi. Baadhi ya watu ni matajiri wakubwa na wamiliki wa makampuni makubwa ndani yao na ndio kusudio la kuumbwa kwao ,ila kwa kushindwa tu kutambua hilo wao wamebaki kuwa masikini na mafukara wakubwa. Lewis Carol, mwandishi mashuguli wa miaka ya 1800 aliwahi kusema Ikiwa haujui unaenda wapi, barabara yoyote itakufikia “. Kwa mtazamo huu mtu asitegemee kupiga hatua ikiwa hajui kusudio la maisha yake ni nini.

Katika mchakato mzima wa kufikia kusudio sahihi linakuwepo ndani ya mtu na uwezekano wa kutimilika kun maswali yanamjuzu mtu kujiuliza na kasha kuanzia hapo ule mchakato mzima wa kuyafikia malengo ya maisha na mafanikio huanzia hapo.

·        Kitu kipi unakihitaji sana?
·        Jambo gani linakufikirisha sana?
·        Kwa namna gani unatumia pesa zako?
·        Namna gani unatumia muda wako?
·        Ni akina nani unafurahi kushirikiana nao?
·        Kipi kinakufanya ucheke?
Mambo haya yapatayo saba ni kichocheo kizuri sana katika kuyafika makusudi ya maisha na  mafanikio. Ni moja ya funguo kubwa katika kufungua makufuli na vifungo na ubongo wa kila mwenye nia thabiti ya kutaka kupiga hatua.Hakuna atakayekua na na mafanikio ya kweli isipokua yule anaefanya kitu ambacho yeye ni shauku (passion) yake kuyafanya.
Ngoja nikwambie, ifahamike kwamba mambo mengi tunayoyafanya si lengo la kuwepo kwetu isipokua kutokutambua tu ndio kunatupeleka katika lengo lisilo sahihi  la maisha na ndio tunalalama na kukosa mwelekeo yaani mbona maisha yamekwama. Baadhi yetu tunaamini tumefanikiwa mbele ya macho ya watu kwa kumiliki vitu vya thamani ila ukweli ni kwamba mafanikio ni zaidi ya hayo.
Kwa maneno yasiyokuwa rasmi mafanikio ni kuwa vile unavyopenda kuwa na kunufaika na kunufaisha wengine kwa vile unavyovipenda. Ukweli ni kwamba wengi tunatumia nguvu nyingi kutafuta vitu ili kuridhia macho ya watu au tu kusongesha maisha mbele, ila pengine hata hatufurahii kile tunachokifanya isipokuwa ni mfumo na msukumo tu wa maisha ndio unatulazimisha kuwepo hapo na hatuna namna.
Hakuna jambo bora sana katika maisha kama kufanya jambo ambalo unalifurahia na linakuletea kipato. Jambo amabalo unaingoja asubuhi ili uamke na kulifanya,jambo ambalo hautamani jua lizame kabla haujamaliza. Na hili ndilo kusudio la maisha linautosheleza moyo ,linatosheleza wengine na linaleta kipato. Kipato hufuata tena kikubwa na kwa kasi kubwa hasa unapofanya jambo sahihi kwa wkati sahihi ambalo ni kusudio la kuwepo kwako.

Upo duniani kwa lengo maalum, ligundue leo!

Kila mmoja katika hii dunia ana lengo na kazi maalumu ya kufanya ambayo hakuna mtu mwingine yoyote aliletwa kuifanya. Kama ambavyo alama za vidole (finger prints) zilivyo tofauti; basi na lengo la kuwepo kwako duniani ni tofauti na la mwingine, japokua kwa mbali sana linaweza onekana linafanana na mwingine.
Kujua lengo au kusudio la maisha yako inakupasa; kujua ni kitu gani unakifanya vizuri zaidi, watu wanapenda nini toka kwako, kitu gani una shauku nacho kila inapoitwa leo. Geuka nyuma na tafakari na kukumbuka.



1.     Ni kitu gani huwa unashauku ya kukifanya na huwa ni kirahisi sana kukifanya hata kama wengine wanakiona kigumu na wanashindwa pengine?
2.     Jambo gani unachukia sana unapoona mtu mwingine anakifanya kwa makosa wakati wewe unaweza kukifanya vizuri sana?
3.     Kitu ambacho unapenda kukifanya hata kama hautalipwa unaendelea kukipenda?

Kuna zawadi kubwa sana ndani yako itafute, ifanye iwepo ikufanyie kazi na uifurahie,itabadili maisha yako na ya wengine na hii ndio njia ya kutafuta na kupata kusudio la maisha yako.
Katika kufikia kusudio la maisha yako fuata hatua zifuatazo itakusaidia.
Hatua ya kwanza: Jenga picha ya kule unapotaka kufika.


Jione wewe uliefanikiwa yaone mafanikio yako. Hii itakusaidia kuongeza jitihada kufikia mafanikio.Picha kubwa hii unaiona katika jambo ambalo unalipenda na kuliweza. Mfano unajiona upo uwanja mkubwa unacheza mpira na timu kubwa Afrika au duniani. Endapo tu unapenda na unajua kucheza mpira. Hii itatoa hamasa ya kufanya mazoezi na kuweka juhudi katika kufikia lengo na kusudio la maisha yako ya mafanikio. Cameron Johnson mzungumzaji na mshauri wa makampuni Zaidi ya 500 makubwa duniani moja ya nukuu zake aliwahi kusema “Usiogope kukataliwa ,usitafute sababu ya kushindwa ,anza kidogo, tia mkazo kufanya mambo mazuri na kila kitu kitafuata .Kila kitu kina kujifunza na mwishowe mafanikio huja kama mfumo wa maisha”.Kikubwa ni kuanza na kufanya katika usahihi utashangaa jinsi mafuriko ya mafanikio yanavyokupata.

Hatua ya pili: Weka nguvu na mkazo katika yale unayotaka kufanya.
Chukua hatua walau ndogo ,thubutu kufanya walau kidogo,weka mikakati na usiogope kujikwaa ama kuanguka. Ni sehemu ya mafanikio kwa maana utakua umejifunza.Kwa kuwa sasa unajua nini unaweza na nini unataka na wewe ni nani.
Kwa kuwa na uhakika na hilo ,sasa unaweza kuchukua hatua maana mafanikio yako yapo ndani yako.Kumbuka ni hatua ya kwanza ndio jambo kubwa Zaidi.Haitatokea miujiza ya kufanikiwa kufikia kusudio la maisha kabla haujachukua hatua yoyote ,kwa kushindwa kufanya hivyo utabaki hapo ulipo na labda utapiga hatua nyuma.

Hatua ya tatu: Songa mbele.
Haijalishi ni ngumu kiasi gani, hakuna jambo zuri lilikuja kwa urahisi. Usiruhusu mawazo ya watu wengine yakubomoe hali ya kua unaamini kile unachokifanya ni sahihi. Kumbuka kila mtu ana historia ya maisha yake. Fikiria nje ya sanduku na amini wewe ni Zaidi ya ulivyo.Tumia akili yako yote na uwezo wako wote kulisimamisha hilo unaloliamini maana hilo ndio wewe.Katika jamii kila mmoja huwa na maoni yake juu ya kila tukio ambalo linatokea. Wapo ambao kwa mawazo yao huamini haitakaa iwezekane jambo Fulani kutokea. Ila kwa kuwa wewe unaweza na unaamini unaweza basi ni kweli unaweza.
Katika jambo ambalo upo mahala sahihi na unatia jitihada basi hata Mungu husimama nyumba yako na kukuandalia majeshi ya kukuvusha salama . Hotuba ya Mwalimu Julius Nyerere aliyoitoa tarehe 2 Novemba, 1978 alipokuwa akitangaza vita vya kupambana na uvamizi wa majeshi ya Idd Amini katika ukumbi wa Diamond Jubilee, alisema kauli ya “…………Uwezo wakumpiga tunao. Sababu ya kumpiga tunayo. Na nia ya kupiga tunayo……..”  kwa kuamini hivi ndivyo ilivyokuwa na ushindi mkubwa ulipatikana. Unapokuwa na nia sababu , na uwezo kwa nini ushindwe?

Hatua ya nne: Weka vipaumbele katika mambo ya msingi.
kila jambo unatakiwa ufanye ,si kila biashara nzuri iliyomletea mtu Fulani mafanikio basi na wewe utapata nalo mafanikio. Tengeneza mtandao wako wa watu na ushirika na watu ambao watakua na wewe katika mchakato. Moja ya mambo niliyowahi kujifunza ni kwamba unapotaka kufika mahala Fulani ikiwa ndio sababu ya uwepo wako basi kuna watu waliumbwa na wao lengo la kuwepo kwao ni kuhakikisha lengo lako linatimia, na kama haujachukua hatua basi kuna idadi kubwa ya watu wanaangukwa kwa wewe tu kutokufanya hivyo.
Wao wanatakiwa kufikia kusudia la maisha yao ila wewe ni sehemu ya kusudio lao kama wao walivyo sehemu ya kusudio lako. Unaweza kuwa na wazo pan asana na pengine wewe pekee usitoshe na unahitaji watu wa taaluma mbali mbali basi hao ndio wa kuwatumia na muweze kusafiri pamoja  kila mtu kufika kusudio la maisha yake. Mwandishi Winston Churchill aliwahi kusema ….tunajenga majengo yetu ,na majengo yetu hutujenga.” Kusudi ya kauli hii ya bwana Churchill ni kwamba kile ambacho tuanakifanya leo ndio picha halisi ya kesho yako.Fanya kazi leo ,tena kwa nguvu sana na kesho utafurahia kwa dhifa kubwa.

Hatua ya Tano: Tengeneza brand ya kusudio lako.
Kumbuka unachofanya ni cha kwako basi kifanye kwa namna yako na si kwa namna ya mwingine kuwa wa kipekee hata kama mwingine anafanya si lazima ufanye kama yeye kwa sababu yeye sio wewe. Be “you”nique.
Jifunze tena na tena ili kujiimarisha kwa unalotaka kulifanya. Kuna tofauti kubwa sana kati ya ukweli wa wewe ulivyo na nini kipo ndani ya watu wanaokutazama.Tengeneza picha yako.

Hatua ya Sita: Endelea kujiboresha leo ,kesho na kila siku.
Usijifunge hapo jaribu kukua na kufanya jambo jipya kila unapotaka au inapohitajika kufanya hivyo. Na mara nyingi unapofanya jambo ililoumbwa kwalo basi utaendlea kufanya licha ya ugumu wowote kaa tulivyosema awali kitu amabacho hata usipolipwa una nraha kufanya. Na hili litatoka kuwa jambo unalolipenda tu mpaka jambo lenye kuleta faida kubwa.Tumia teknolojia ni msaada mkubwa Kuwa mbunifu Kwa hatua hizi kwa kuwa na ustahimilivu na jitihada itapelekea mafanikio kutokea kwa wakati. Ama ni biashara au aina yoyote ya shughuli ya kupata kipato basi ona kwamba hilo ni jambo lako na ndilo unalopaswa kulifanya ndilo unalolimiliki.
Usiwe mzito katika kufanya maamuzi, kutumia taarifa zinazopatikana hata kama ni ndogo, matumizi ya muda jua ni wakati gani wa kusema NDIYO au HAPANA au KUKAA KIMYA. Jua ni wakati gani wa kujifunza, kuondoa mawazo hasi kichwani ,wakati wa kutafakari na kutafakari tena na tena.Kujiboresha ndio msingi wa kufika kusudio la maisha yako.
Kwa maneno ya Siddhārtha Gautama,mwanafalsafa ,mwalimu na kiongozi ya dini ya kibuddha "Kusudio lako maishani ni kupata kusudi lako na kutoa moyo wako wote na roho yako yote kwenye kusudio hilo"
Siddhārtha Gautama



……………………….
Mwandishi ni mkurugenzi wa Umoja Creatives Company na Mkufunzi wa Uongozi na Menejimenti. Mawasiliano: +255 716 050 555, +255 754 686 393, abbshey09@gmail.com
                                                            …………………………..

No comments:

Post a Comment