Monday, March 19, 2018

Nguvu ya Asante

Unaijua nguvu ya asante?
Katika kipindi cha ukuaji tangu tuwapo wadogo, kati ya maneno ya mwanzo kabisa kujifunza ni kusema asante. Je hukuwahi kujiuliza kwa nini wazazi au walezi hukazia hapo na kutaka mtoto ajue kusema asante? Pengine hata wao hawajui,kutakua na fumbo kubwa sana ndani yake.
Nini maana ya asante ?
Pengine ni neno ambalo ni la kawaida sana na ambalo tunalitumia mara kwa mara pale ambapo tunakua na lengo la kuwasilisha hisia njema juu ya mambo tunayofanyiwa ama kupewapo. Upana wa neon asante msingi wake ni kuelezea kujali,kutambua thamani,heshima,shukrani, na mengi ya kufanana na hayo.
Kila binadamu hata akiwa ni mkatili au mkaidi wa kiasi gani,huona fahari kusikia maneno mazuri ikiwa ni pamoja na asante hata kwa dogo alilolifanya akiamini kuwa ni jema ,hapa ataona thamani na kuheshimiwa kwake. Katika nyakati za ugumu neno asante hudumisha uhusiano na mwendelezo wa mambo mema baina ya watu ama makundi ya watu.
Katika utamaduni wa watu wa magharibi tangu miaka ya 1800 wamekua na siku maalumu kwa ajili ya kusheherekea asante wakiita kama “thanksgiving”. Kwa kuuona umuhimu wa asante imekua ni utamaduni wa kudumu na umerithishwa vizazi na vizazi. Sherehe hizi zimekua zikisheherekewa kwa watu kukaa pamoja na familia au jamaa na kuzungumza pamoja na kupeana shukrani kwa mambo mema yaliyotokea katika kipindi cha mwaka mzima, kula chakula kwa pamoja , kucheza pamoja na pia kufanya shughuli mbalimbali kwa pamoja.
Kwa kufanya hivi imekua ikileta athari njema kwa familia na koo zao kwan hudumisha umoja na ushirikiano wa kifamilia na kusuluhisha migogoro endapo ilitokea.
Katika utamaduni wa kiafrika imekua kawaida kujifunza na kusema asante japo utamaduni huu unazidi kuathiriwa siku hadi siku kutokana na sababu mbalimbali ambazo tunaweza kuzirejea kama si sababu za msingi. Moja ya mambo yanayodidimiza utamaduni huu ni aina ya malezi ambayo yamekua yakitolewa na wazazi wa kizazi hiki kwa kuamua au kusahau kutilia mkazo juu ya kusema asante. Pengine kwa sababu tu tumekua tukijifunza na tukifundisha kusema asante kwa sababu ni utamaduni tuliorithishwa na wazazi au ni jambo tu la kawaida ambalo huwa tunalifanya na kuona ni la kawaida tu kama maneno mengine.
Kuna haja ya kwenda mbali zaidi na kutizama je kuna umuhimu wa kusema asante na kwa nini tunasema asante.
Athari za neno asante.
Neno asante lina uwezo la kuhamasisha na kutia nguvu ndani ya watu. Umewahi kufikiri juu ya mtoto anaetumwa na mama yake akalete chombo ndani ama kwennda dukani na sokoni kununua bidhaa fulani kisha mama akamwambia asante? Pengine angeweza kumtuma mara nyingi zaidi bila ya mtoto kuona kama amesumbuliwa, angeweza kwenda tena na tena kwa kuona tu mama anatambua mchango wake au utendaji wake.
Hivyo hivyo pindi anapopokea mtu msaada na kasha akasema asante , basi atakaetoa msaada anaona wazi kabisa kuwa amefanya kitu cha thamani na ataona umuhimu wa kufanya tena na tena.
Utafiti uliofanyawa na chuo cha Georgia nchini Marekani juu ya masuala ya ndoa kauli ilitolewa na watafiti ilisema “tumegundua kwamba kutambua thamani ya mwenzi wako kwa kumshukuru kwa kila jambo,inaongeza nafasi ya kudumu kwa muda mrefu na kuona kwa kiasi gani pande mbili katika ndoa zimeivaa ndoa vilivyo”. Hii inamaana ataweza mtu kuvumilia zaidi na zaidi ndani ya ndoa yake kwani thamani ya mema anayoyafanya yanaonekana na kutambuliwa.
Kushindwa kusema asante
Kushindwa kusema asante kunapelekewa na mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuona ya kwamba tumeridhika,ubinafsi,ukosefu wa malezi bora, kujiona ni bora zaidi ya wengine na kadhalika.
Kushindwa kusema asante humfanya mtu kuonekana ana majivuno na kiburi. Mahusiano baina ya watu huathirika kwa kushndwa kusema asante. Hatafanya mtu jambo kubwa au hata dogo akaona kafanya pasito na watu au mtu kutambua amefanya kitu.
Katika kuboresha maisha yetu na vizazi vyetu busara zaidi kjifunza kusema asante hata kama si jambo kubwa au kitu kikubwa ambacho tunapewa.Mahusiano baina yetu utu na uungwana ni matunda yatakayotokana na kujifunza na kusema asante kwa dhati.
Asante ya dhati
Kuna namna mbali mbali za kufanya asante kuwa na sura ya dhati na iweze kuleta uchanya pale ambapo inatolewa . kwa mapendekezo hizi ni namna bora za kusema asante ya dhati.
Iseme kwa lengo mahususi.
Kusema asante tu bila kusema asante inahusu nini ni jambo unalolishukuru.Mfano “mama, asante sana kwa kuninunlia zawadi ya kitambaa nimeifurahia sana” hii itamgusa moja kwa moja alieshukuriwa na kuona uzito na thamani ya kile ambacho amekifanya na ataona munganiko na furaha ndani yako. Isisemwe asante inayoning’inia na kuacha maswali ya hasa nini mtu anashukuru? Kwa kiasi gani asante umeguswa na wema uliotendewa.
Ushiriki wa mwili na viungo
Kusema asante hali ya kuwa umenuna au ukiwa na kisirani haiwezi kuwa asante ya dhati. Ni vyema unaposema asante umaanishe na mwili mzima onyesha muunganiko wa asante na mwili wako na uso uoneshe ya kuwa unamaanisha. Vitendo husema zaidi ya maneno, hivyo itende asante yako na ionekane.
Chagua mahala na muda sahihi
Wakati unataka kusema asante sharti kuchagua mazingira sahihi ya kusema asante, Si mahala popote unaweza kusema asante. Iseme wakati inatakiwa kusemwa kisipite kipindi kirefu kabla ya kusema asante kwa wema uliotendewa leo.
Ili kupata zaidi tukumbuke kusema asante na tuwakumbushe wengine kusema asante, Makuzi kwa watoto wetu yaambatane na kujifunza kusema asante pia tuseme asante ya dhati na si asante ya juu juu kwa maana tumaanishe tusemapo asante.
Kumbuka “Mara nyingi huwa tunakumbuka sana pale mtu anaposahau kusema asante ,hasa ambapo umetumia muda na nguvu kumsaidia , hapo ulipo umekumbuka tukio kama hilo”
Imeandaliwa na Abdallah Wihenge

2 comments:

  1. Jibu la asante huwa ni nini?

    ReplyDelete
  2. Inategemea na utamaduni wa watu.Ila ni vema kuonesha umefurahishwa na mrejesho wa namna yoyote walau kusema "asante kushukuru"japo si jibu rasmi.

    ReplyDelete