Tuesday, November 1, 2022

Urithi wa umaskini

Mathalani watu wachache wanaweza wasijue kama ambavyo utajiri unarithishwa basi ni hivyo hivyo kwa umaskini, ndiyo umaskini unarthishwa kutoka kizazi kwenda kizazi laba kwa kujua kwa kutokujua basi jamii hurithishana umaskini.

kama una kumbukumbu nzuri za namna matajiri huwarithisha watoto na vizazi vyao utajiri basi ni hatua zilezile pia maskini huzitumia kuwarithisha watoto na vizazi vyao. Mtizame tajiri wa migodi pale Mererani ,pengine atamchukua moja ya mwanafamilia yake na kwenda nae japo kutizama ni kwa namna gani madini yanapatika kwa kila hatua, atamhubiria juu ya namna ambavyo ataweza kunyakuka kimaisha endapo atafanya juhudi na kutumia maarifa sahihi kuyafikia madini, atasaidia kuonesha ugumu na urahisi wa kuayafika malengo na kubwa zaidi ataonesha mfano wa mafanikio japo kwa mtazamo wa maisha yake na vile anavyovimiliki.

Mfano huu utampa kiu ya mafanikio au hamu ya kumiliki mali mlengwa. Japo hatuhesabu pesa kama mafaninikio ila ni kiungo katika viungo muhimu vya mafanikia hilo halikwepeki. Pengine kwa miongo kadhaa mwanafamilia huyu atatamani naye aanze kufanya jambo japo kwa udogo ili kunyanyua hatua na atafanikiwa. Hata kama hili halitafanikiwa ataweza pata msukumo wa kufanya jingine lengo tu kufika pale ambapo tunaamini ni kiu ya kipato.

Mara kadhaa familia zenye utajiri hasa wa kipato huwa ni mfano mzuri kwa vizazi vyao, licha ya yote lakini maongezi na matendo yanayoendelea katika familia kwa kiwango kikubwa yatasadifu na kufunza utajiri.

Yote hayo yanategemea sasa tajiri huyu wa kipato ametokea wapi na je amelelewa katika namna ya kipato?Ni maswali mepesi sana ambayo yatafikirisha endapo mtu angetaka kufikiri. Ni mara chache sana kwa aina ya watu waliolelewa kimaskini (sio maskini) kuishi maisha ya kitajiri kuanzia nafsi na matendo. Changamoto nyingi zinazikumba jamii zetu hasa za kiafrika kuaminisha kwamba umaskini ni sifa au ni unyonge na udhaifu. Mathalani utamsikia mzee alielelelewa maisha duni akisema ''Ona vijana wa sasa ni wavivu sana,zama zetu tulikua tukitembea mpaka kilomita ishirini kutafuta maji ila ninyi umbali kidogo tu mtataka kupanda gari''. ukweli ni kwamba kutembea umbali kwa muda mrefu si jambo jema hasa endapo shughuli au jambo husika linapaswa kufanywa kwa haraka. Kwa ajili ya maendeleo na mapinduzi ya kisayansi na kiuchumi mambo mengi yamerahisishwa na ndio maana ya maendeleo. Hatupaswi kuishi zama hizo wala kuvifanya vizazi viishi zama hizo. Vilevile si vema kuuhubiri umaskini kama jambo la kujisifu au jambo bora ni busara kuukana na kuuepuka.

Kama mzazi au mlezi katika familia anapaswa kuhakikisaha kwa familia inapata mahitaji muhimu kwa kadiri ya uwezo wake huku akiendelea kuulani na kujaribu kila namna ya kuuepuka umaskini. Pengine wengi hawana uwezo wa kuwapatia watoto wao kila ambacho wanakihitaji ,na wengine huenda mbali hata kile kidogo alichonacho pia hatokitoa kwa familia kwa kusema kwamba ''mbona sisi tuliishi maisha magumu''. Si busara kuyaletekeza mabaya ambayo pengine yalikua ni sehemu ya historia ya mtu binafsi na kuyapeleka vizazi vya mbele,ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha familia yake inaishi maiisha bora na ya stara kwa kadiri yake.

Katika mzunguko wa maisha pengine ukakutana na mtu wa makamo mwenye uwezo na kipato na anagombania chakula kidogo, pengine ukakutana na mtu ambaye hapendi kuona wenzie wakipata walau kwa uchache atafanya kila hila kulikwamisha. Endapo utafuatilia hili utakuta pengine mtu huyu alilelewa kimaskini kwa kuoneshwa ugumu wa maisha na kwamba kila mmoja lazima apitie magumu hata kama ugumu hakuna.Jambo hili linapelekea kupatikana kizazi cha watu wachoyo,wenye husda na visasi kupitiliza.

Ieleweke kwamba umaskini ni jambo ambalo yeyote katika watu anaweza kunasibiana nalo na hakuna anaependa kuwa nalo,rai ni kwamba hatupaswi kuhubiri umaskini kama jambo sawa katika maisha ya mwanadau au kuishi katika hali ya umaskini hata kama hapana haja ya kufanya hayo kwani ndio maana halisi ya kurithisha umaskini.

Tukutane katika makala ijayo ili kuendelea kujengana.

Imeandaliwa na:

Abdallah Wihenge 

Mkufunzi wa masuala ya kitaasisi na tabia



No comments:

Post a Comment