Sunday, May 10, 2020

Si lazima ufanye kila biashara


Imeandikwa na Abdallah Wihenge 

Kutokana na changamoto za ajira ambazo  zinazikumba nchi nyingi hasa  za ukanda wa Afrika pengine na maeneo mengi duniani ,pamekua na mihehemko hasa kwa jamii maskini juu ya kujikwamua kutoka katika wimbi la ukosefu wa ajira na kipato.

Changamoto hii imepelekea wengi katika vijana pengine na watu wengine wakijikuta kwa kupapasa tu na bila kutumia nyingi katika fikra zao kutafakari juu ya nini na wakati gani wafanye nini. Suala hili limepelekea watu wengi kujikuta kila fursa au inayoitwa fursa basi na yeye ataingia kwa kiu tu ya kupata kipato au ujira ili kujikwamua kitoka kaika wimbi la umasikini.

Katika makala hii nitagusia maeneo kadhaa katika utimamu wa kuchagua fursa za kibiashara na kijarisiamali. Na ikumbukwe kwamba kila mtu ana kusudi katika maisha kwa maana sababu ya kuwepo kwake, na ndio maana binadamu wote hawawezi kufanya kila kitu na kila jambo. Hii ina maana hatokuwepo mtu wa kuwa mwalimu yeye, daktari, mkulima, mvuvi, mkandarasi kwa wakati mmoja..

Katika makala zilizozopita zilieleza wazi juu ya kusudi la maisha , na ni kupita makala hizo na nyinginezo utajua nini kusudio la maisha yako na kuanzia hapo utapata njia ya kusonga na kupiga hatua katika maisha kwa kujua wewe ni nani na unataka kufanya au unatakiwa kufanya nini duniani.
Katika harakati za kujikwamua kila mmoja ana namna ya kipekee ambayo anaitumia kuelezea namna ya kujikwamua.Mathalani  yapo makundi yanaamini katika biashara ya mtandao na faida zake katika kujikwamua,wapo watu wanaamini juu ya biashara ya kilimo na mazao na wanaijua jinsi ilivyo, biashara ya udalali ,vifaa vya umeme na nyingine nyingi.
Hizo zote ni biashara nzuri ila ikumbukwe kwamba si kila biashara ni ya kila mtu kuifanya,hata kama ni rahisi kiasi gani. Zingatia mambo yafuatayo unapochagua aina ya biashara ya kufanya.

  • Haijalishi ni ushawishi kiasi gani unapewa na mtu au mtu juu ya kufanya biashara husika.Fanya kile ambacho unakiamini hata kama hakuna anaekiamini.Kuna watu wana uwezo mkubwa sana wa ushawishi na kutia moyo hata kukufikisha pahala ukaona upande chanya wa jambo na kujikuta unaingia.Ushawishi hasa kwenye jambo la kibiashara ni vyema sana ila washawishi wanapaswa kujua kwamba watu wanatofautiana kati ya mtu mmoja na mwingine.
  • Ili uweze kufanikiwa katika jambo lolote ama ni zuri au baya ,hatua ya mwanzo kabisa ni kuliamini kutoka ndani ama kwa kuambiwa ama kwa kulitafakari mwenyewe.Isitoshe tu kupokea ushawishi kutoka kwa watu na ukakubali eti kwa kuwa umeambiwa ni zuri,kumbuka kuchukua muda wakao kulitafakari na kujiuliza maswali na majibu juu ya uhusiano wake na kusudio lako.
Wengi wamejikuta wakiangukia katika kila biashara na kupoteza pesa kwa changamoto ya kuparamia na ushawishi wa hali ya juu katika biashara fulani fulani.Mfano katika miaka ya hivi karibuni wakina dada wengi waliopo kwenye ajira rasmi na wale waliojiajiri wamejikita katika biashara ya mikoba na vipodozi. Ni biashara nzuri ndiyo ,Ila wengi waliojikita katika biashara hii ni kutokana na msukumo kutoka kwa marafiki pia na mitandao.Hii inapelekea katika sehemu moja ya kazi pengine yenye watu kumi basi watatu wanafanya biashara inayofanana jambo ambalo linapelekea kujidumaza kibiashara na kipato pia kwani mzunguko wa wateja ni ule ule.
  • Pia mlipuko wa biashara ya mtandao ya kwamba, njoo na mtu utapata kiasi fulani kwa uwepo wake. Hii ni moja ya biashara nzuri pia na inafanyika maeneo mengi duniani.Changamoto ni kwamba waelezeaji wa biashara hii huelezea upande mmoja tu wa biashara ,upande wa kupata na wanaacha changamoto na madhira yake nyuma.Ni vema kabla ya kuingia katika bishara hii mbali na ushawishi na msukumo mkubwa kupata muda wa kutafakari na kujiridhisha na kujifunza kwa waliowahi kufanya katika meneo mengine na walifanikiwa kwa kiasi gani.

Wengi wamepoteza pesa na wengi wapo kwenye mapambano ya kurejesha kiasi cha pesa walichowekeza bila kujua hatma yake.Wengi hujikuta wanakomaa na kuendelea kupambana na kuupoteza muda kwa kutaka kuhakikisha kiasi cha pesa kinarejea na anaendendea kupoteza fursa nyingine kutokana na mkwamo huu huu. 

Ni hivyo hivyo katika biashara nyingine kama kilimo, ufugaji, uwekezaji na kadhalika. Si vibaya kushindwa kwani ni kujifunza ila kushindwa katika jambo amabalo haukuiruhusu akili yako kutafakari ni kushindwa kiwango kibaya zaidi.
  • Usichague biashara kwa kigezo cha kujipatia pesa (nyingi) tu.Ni kweli misukumo mingi ya watu juu ya kufanya biashara ni kuhakikisha wanapata pesa za kujikwamua kiuchumi tu.Biashara au shughuli unayoifanya inapaswa kukupelekea kupata kipato cha kujikwamua ,ila jambo hili likibaki kama ndio lengo kuu na la pekee la kufanya biashara husika, basi kwa asilimia 50 tegemea kutofanikiwa na kuanguka.Wengi waliingia kwenye biashara kwa kushawishiwa na uchu wa kupata pesa. Pesa ni zawadi inayokuja baada ya kufanya jambo jema na sawa, na baada ya kufikia kusudio la maisha yako.Unaonaje kupata pesa kutoka katika kitu au biashara unayoifurahia? Utajisikaje kupata pesa katika jambo ambalo unaona asubuhi inakawia kufika ili ukafanye?Unaonaje kuutumia usiku na mchana wote kufanya kitu ambacho unakipenda na kinakuletea pesa zinazoyafanya maisha yako?
Hii ndio tafsiri ya aina ya biashara na shughuli ya kukupatia kipato unayopaswa kuifanya.

  • Jamii hasa vijana imejikuta katika wimbi la kufanya biashara kwa ajili tu ya kujionesha kwa watu kwamba nao hawajakaa bure kuna biashara ‘mishemishe ‘ wanafanya mjini.Jambo hili linapelekea kujikuta wameangukia kwenye biashara yoyote ,na hatma yake ni kuanguka na kushindwa kujikwamua kiuchumi. Hakuna anaejali ni nini unafanya hali ya kuwa hakina manufaa au hakina tija kwako au kwa jamii yako. Unahitaji kukaa chini  kutafakari na kuchanganua chochote ambacho unakitizamia kukifanya ili kikuletee kipato.Ni ngumu kufanikiwa katika jambo usilolijua ama kwa bahati nasibu ambayo nayo haitakuja mpaka uwe katika mazingira ya kuipata bahati.

  • Kuiga toka kwa watu, Hili pia ni janga kubwa hasa kwa jamii ya wazawa wa ulimwengu watatu. Mathalani elimu tuliyoipata na jamii tulizotokea hazikutuandaa kuweza kufanya maamuzi ya biashara gani au shughuli gani ya kipato yatupasa kuifanya. Hii inapelekea kuiga kwa ‘sisisi’ kutoka kwa watu wanaofanya aina fulani ya biashara. Mfano bwana fulani alifanikiwa kwa biashara ya duka la rejareja mtaani kwake , na kijana mwingine wa mtaa mwingine akaona mafanikio hayo na agharabu ana mtaji wa kumuwezesha kufanya aina hiyo ya biashara husika basi bila ya kufanya tafakari kwa yakini ,anachokitizama mbele yake ni mafanikio na sasa anakwenda kujikita katika biashara hiyo , na pengine katika mazingira yasiyo sahihi ama mbinu zisizo sahihi na anaanguka. Ni vema kujifunza na kujihakikishia juu ya kile unachotaraji kukifanya.

  • Maamuzi ya biashara moja kwa wakati mmoja ni bora zaidi kwa kuanzia.Changamoto nyingine inayowagharimu watu wengi ni kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja.Utaona ajabu unakutana na mtu ndani ya mwezi mmoja ameshafanya takribani biashara tatu na mbili zilikwishashindwa na moja ndio anayoifanya na inaelekea kushindwa.Pengine ni tamaa au shauku ya kufanikiwa ndio msukumo wa hadha hii.Moja ya jambo kubwa ni kuweza kuwa na uwezo wa kusimamia akili binafsi.Kufanya biashara nyingi kwa wakati mmoja inapelekea kukosa kumakinika katika wazo moja la biashara na pengine maisha kwa ujumla. Kutumia muda mwingi kupigania wazo moja ni bora zaidi ya kuutumia muda huo kufanya mambo mengi yasiyo na tija.

  • Kujijengea uwezo wa kuyachanganua na kuyafanyia kazi maudhui ya wahamasishaji “motivational speakers”
Hawa ni watu muhimu sana na wamekuwa ni msaada mkubwa sana katika kutia chachu ya kuwaamsha watu katika suala zima la maendeleo na kujikwamua, pia ni wazi kwamba wao hufanya shughuli zao kwa makundi ya ujumla hali ya kuwa uwezo wa uchanganuzi na uelewa wa watu unatofautiana.Watu wengi husikiliza maudhui yanayokuja mbele zao hasa juu ya masuala ya biashara na kwa sababu wamehamasika basi hunyanyuka na hamasa na kufanya maamuzi ya kufanya chochote katika biashara, na pale hamasa inaposhuka anajikuta kumbe alichagua biashara kwa mihehemko ya hamasa na alisahau kuushirikisha ubongo wake katika maamuzi. Ni vema kuweka nukta na kutafakari kwa kina kila ambacho unahamasishwa nacho na baadae kuamua maamuzi ambayo hautajutia. kabla ya kuamua maneno mazuri ya wahamasishaji:
1.      Sikiliza na kwa makini maudhui yao
2.      Tenga muda wa kutafakari na kuamua
3.      Amua kwa moyo mmoja maamuzi yaliyo sahihi.

Changamoto nyingi katika maamuzi ya biashara ni shinikizo la hali ya maisha. Ni wazi kabisa uchumi wa dunia umekua na shinikizo kubwa kiasi cha kwamba walio na mawazo makali na mawanda mapana ya kufikiri ndio wanaweza kupambana na shinikizo hilo na kufanikiwa kimaisha hasa kupitia biashara,wenye mawazo legelege na wasiotaka sulubisha akili zao wamebaki kutizama na kubeza au kuamini kwamba kuna watu maalumu wa kufanya mambo ambayo wao wangeliweza yafanya.

Tofauti na miaka ya nyuma kufanya biashara katika zama hizi kunahitaji akili nyingi na maarifa makubwa ya kuweza kufanikiwa.Haitoshi tu kuuza na kununua kama ilivyokuwa zamani, dunia ya sasa namna ya kuuza imekua ndio kigezo kikubwa  cha kufanikiwa katika biashara na kisha bidhaa na ubora hufuata. Ndio maana utaona kuna watu wana bidhaa zisizo na ubora ila wana mauzo makubwa ,na ukweli ni kwamba wanatumia maarifa makubwa sana kuuza na kupenya katika masoko ,bila kusahau ujuzi na maarifa juu ya aina ya biashara wanayoifanya. Hautaweza kufanikiwa kwa kuparamia biashara yoyote isipokua kwa biashara unayoifahamu kwa mapana.

Pamekua na aina fulani ya watu ambao wao hufanya biashara inayo ‘trend’. Hili ni jambo zuri na ni fursa pia.Kufanya biashara ambayo inahitajika kwa wakati huo ni njia nzuri ya kukusanya kipato kwa ajili ya biashara ambayo utaishi nayo.Changamoto ya biashara za namna hii ni kukutoa katika mstari wa biashara yako ya kudumu.Hii inapoteza malengo yako ya muda mrefu na kujikuta unakwenda kutumia nguvu,akili na mali nyingi kupambana na jambo la msimu na kisha baada ya hapo unarudi kuanza moja katika biashara ya kudumu.Mara nyingi biashara hizi hufanywa na kila mtu na faida yake huwa ni ndogo ukilinganisha na rasilimali zitakazowekezwa.

Muda ni mali na ni vyema kuutumia kuboresha jambo kuu la msingi kuliko kushughulika na mambo madogo madogo yanayotumia rasilimali muda zaidi.
Katika Makala zitakazofuata tutatizamia namna gani ya kuanza kidogo katika biashara kwa kutumia mtaji kidogo na maarifa mengi,